6 Mei 2021 - 10:13
Mashirika ya Kimataifa: Mamilioni ya watu wanakabiliwa na baa la njaa duniani

Imeelezwa kuwa, kuna idadi kubwa na inayoongezeka ya watu wanaokabiliwa na njaa kali na wanaohitaji msaada wa kuokoa maisha katika maeneo mbalimbali ya dunia.

Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Hayo yamo katika ripoti ya kila mwaka iliyozinduliwa kwa pamoja na muungano wa kimataifa wa Umoja wa Mataifa, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kwa ajili ya kushughulikia mgogoro wa chakula.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, idadi kubwa ya watu wenye njaa kali katika nchi zilizokumbwa na machafuko ilifikia kiwango cha juu zaidi katika miaka mitano.

Ripoti hiyo ya “Mtandao wa kimataifa dhidi ya mgogoro wa Chakula” inaonesha kuwa, watu wasiopungua milioni 155 walikabiliwa na ukosefu mkubwa wa chakula katika viwango vibaya zaidi vya daraja la 3 katika nchi na maeneo 55 kwa mwaka 2020.

Mtandao huo wa kimataifa unaojumuisha Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na Umoja wa Ulaya (EU) umesema kuwa, “hii inawakilisha ongezeko la karibu watu milioni 20 kutoka mwaka uliopita, na ni uthibitisho kwamba hali mbaya ya ukosefu mkubwa wa chakula imekuwa ikiongezeka kwa kasi zaidi katika miaka mitano iliyopita.”

Mwaka mmoja baada ya janga la corona au COVID-19 kuenea ulimwenguni kote, toleo la mwaka 2021 la ripoti ya kimataifa juu ya mgogoro wa Chakula inathibitisha kuwa, janga hilo na hatua zinazohusiana za kudhibiti kusambaa zaidi zimesababisha athari mbaya zaidi kwa changamoto ambazo tayari zilikuwepo hususan mizozo na mabadiliko ya tabianchi.   

342/